Katika kauli inayothibitisha wazi mipango ya kufanya mabadiliko haramu ya kijiografia na idadi ya watu, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ametangaza kuwa hakuna suluhisho la kudumu kwa Ukanda wa Gaza bila ya kufukuzwa kwa mamilioni ya wakazi wake.

Akizungumza kuhusu mkakati huo, Katz alidai bila uthibitisho wowote kuwa tafiti zinaonyesha asilimia 80 ya Wapalestina wanataka kuondoka Gaza, akisisitiza kuwa jeshi la Israel liko tayari kutekeleza ufukuzaji huo kupitia njia za bahari na anga mara tu mazingira yatakaporuhusu, hasa baada ya Misri kukataa katakata kuruhusu mpango huo kupitia ardhi yake.

Waziri huyo alifichua kuwa nchi zilizokuwa tayari kuwapokea Wapalestina hao zinashikilia sharti la kupata uungwaji mkono na hakikisho la serikali ya Marekani. Aidha, alibainisha kuwa Rais Donald Trump hakufuta mpango huo bali aliusimamisha kwa muda kufuatia shinikizo kali kutoka kwa viongozi wa mataifa ya Kiarabu.

Hata hivyo, Katz alionya kuwa utekelezaji kamili wa mpango huo ni suala la muda, akisema: “Wakati utafika pale itakapobainika wazi kuwa Hamas haitekelezi wajibu wake. Ndipo tutakapopata idhini kamili ya kusonga mbele kijeshi, kimipaka, na katika maeneo mengine, na jambo hili litapata kasi kubwa.”

Matamshi haya yamezua taharuki mpya kikanda, yakidhihirisha mwelekeo wa Tel Aviv wa kutaka kubadilisha kabisa mustakabali wa eneo hilo kupitia ufukuzaji na uhamishaji wa kulazimishwa.

Leave a Reply