Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright, ametoa kauli mpya za vitisho dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisisitiza kuwa Washington iko tayari kutumia njia yoyote—ikiwemo nguvu za kijeshi—kuzuia kile alichokiita upatikanaji wa silaha za nyuklia na kusitisha mpango wa nyuklia wa Tehran.

Akizungumza siku ya Jumatano, Wright alieleza kuwa utawala wa Marekani unataka kukomesha shughuli za nyuklia za Iran kupitia mazungumzo na ukaguzi mkali wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), au vinginevyo kwa kutumia nguvu. Matamshi hayo yamepuuza haki ya kisheria ya Iran chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) wa kutumia nishati ya atomiki kwa malengo ya amani.

Wachambuzi wa masuala ya kijiopolitiki wanaona kauli za waziri huyo kama jitihada za kupunguza hasira za wananchi wa Marekani wanaokabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei ya mafuta na nishati, uliosababishwa na taharuki za kijeshi na changamoto za kiusalama katika Mlango-Bahari wa kimkakati wa Hormuz. Tehran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani na kwamba lugha ya vitisho haitafanikiwa kuilazimisha kusalimu amri.

Leave a Reply