WASHINGTON, MAREKANI — Ripoti ya gazeti la The New York Times imeeleza kuwa Wizara ya Vita ya Marekani inakabiliwa na msukosuko mkubwa wa uongozi baada ya kufukuzwa kwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu, hatua inayodaiwa kusababisha pengo katika mfumo wa uongozi wa Jeshi la Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegseth amefanya mfululizo wa mabadiliko katika uongozi wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na kumuondoa Jenerali Randy George, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu ya Marekani.
Baada ya kuondolewa kwa Jenerali George, jeshi limekuwa bila Mkuu wa Majeshi wa kudumu kwa kipindi cha miezi kadhaa, hali inayozua wasiwasi kuhusu uthabiti wa uongozi wa taasisi hiyo.
Ripoti hiyo inasema Hegseth pia amewaondoa angalau maafisa wakuu watatu ambao walitarajiwa kuwa miongoni mwa wanaoweza kurithi nafasi ya Jenerali George.
Kwa mujibu wa maafisa walionukuliwa, Waziri wa Jeshi Daniel P. Driscoll pia anatarajiwa kuondoka serikalini katika miezi ijayo. Hali itakayodhoofisha zaidi Jeshi la Marekani.
Muktadha
Mabadiliko hayo ya uongozi yanakuja wakati Marekani ikiendelea kukabili changamoto nyingi za kiusalama duniani, ikiwemo migogoro Mashariki ya Kati baada ya uvamizi wake dhidi ya Iran, ushindani wa kijeshi na China, pamoja na vita vinavyoendelea kuhusisha washirika wake kama vile Ukraine.
Wakosoaji wanasema kuondolewa kwa maafisa wengi waandamizi kwa muda mfupi kunaweza kuathiri mwendelezo wa mipango ya kijeshi na utendaji wa jeshi.
Hata hivyo, wanaounga mkono mabadiliko hayo wanadai kuwa ni sehemu ya juhudi za kurekebisha mfumo wa ulinzi na kuhakikisha uongozi unaendana na sera mpya za serikali ya Donald Trump
Athari
Iwapo pengo la uongozi litaendelea, wachambuzi wanaonya kuwa linaweza kuathiri uwezo wa Jeshi la Marekani kupanga mikakati ya muda mrefu na kufanya maamuzi ya haraka katika kipindi cha migogoro ya kimataifa.