BEIJING, CHINA – Juhudi za kidiplomasia za kuleta utulivu kati ya mataifa hasimu ya Iran na Marekani zimechukua mwelekeo mpya, huku kukiwa na ishara za wazi kuwa nchi hizo mbili zipo ukingoni mwa kufikia makubaliano rasmi.

Taarifa hizi zimefichuliwa na Shirika la Habari la Rasmi la China (Xinhua), likiripoti kuhusu mazungumzo ya faragha na ya ngazi ya juu yaliyofanyika mjini Beijing kati ya Rais wa China, Xi Jinping, na Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Jenerali Asim Munir.

Katika mazungumzo hayo, Jenerali Munir—ambaye amekuwa akitekeleza jukumu la upatanishi—alimfahamisha Rais Xi kuwa mchakato wa maridhiano kati ya Tehran na Washington umepiga hatua kubwa na sasa upo katika hatua za lala-salama.

“Makubaliano kati ya Iran na Marekani sasa yamekaribia kukamilika. Pande zote mbili zipo katika hatua za mwisho za kufikia muafaka wa kudumu,” alinukuliwa Jenerali Munir.

Mkuu huyo wa jeshi la Pakistan aliwasili Beijing moja kwa moja akitokea jijini Tehran, safari inayoelezwa kuwa na lengo la kutoa mrejesho wa mwisho kwa uongozi wa China kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika meza ya mazungumzo.

Hatua hii inatazamwa na wachambuzi wa mambo ya kimataifa kama ushindi mkubwa wa kidiplomasia, huku Pakistan na China zikionekana kuwa na mchango mkubwa katika kuzipatanisha nchi hizo ambazo zimekuwa na uhusiano wa kusuasua kwa miongo kadhaa.

Ingawa maelezo ya kina ya makubaliano hayo bado hayajawekwa wazi, ripoti hii inatoa matumaini mapya ya kupungua kwa mivutano ya kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Mashariki ya Kati na duniani kote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *