Kampuni ya utayarishaji wa filamu ya Universal Pictures, kwa kushirikiana na mwongozaji mahiri Michael Bay, imetangaza mipango ya kuandaa filamu mpya itakayoelezea kisa cha kusisimua cha uokoaji wa marubani wawili wa Jeshi la Anga la Marekani nchini Iran.
Kwa mujibu wa jarida la Deadline, tukio hilo lilitokea kufuatia kudunguliwa kwa ndege yao aina ya F-15E Strike Eagle wakati wa Operesheni iliyopewa jina la “Epic Fury.”
Filamu hiyo inatarajiwa kuakisi maudhui ya kitabu kipya cha mwandishi Mitchell Zuckoff, kinachotarajiwa kuchapishwa mwaka wa 2027.
Akizungumza na Deadline, Michael Bay ameeleza kuwa anatarajia ushirikiano wa karibu na vyombo vya ulinzi vya Marekani, akibainisha kuwa amekuwa na uhusiano mzuri wa kikazi na Idara ya Vita pamoja na wanajeshi wa Marekani kwa miaka mingi. Kauli hii imezua hisia kuwa mradi huo unaweza kupata ridhaa na ushirikiano wa moja kwa moja kutoka Pentagon.
Bay amesisitiza kuwa filamu hiyo itatoa heshima kwa wanajeshi waliofanikisha operesheni hiyo, ambayo ameitaja kuwa ni miongoni mwa misheni ngumu, tata, na zenye hatari kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni ya kijeshi.
Hadi sasa, maelezo zaidi kuhusu waigizaji au tarehe kamili ya kuanza kwa utayarishaji hayajawekwa wazi.