Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ametangaza kuwa mataifa ya Urusi na China yameacha kabisa kutumia Dola ya Marekani katika mabadilishano yao ya kibiashara.
Badala yake, Lavrov amesema kwa sasa nchi hizo mbili zinafanya miamala yao yote kwa kutumia sarafu zao za kitaifa, yaani Ruble ya Urusi na Yuan ya China.
Akiendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu masuala ya kiusalama, Lavrov amegusia mzozo unaoendelea nchini Ukraine, akisisitiza kuwa Urusi imedhamiria na itahakikisha inafikia malengo yake yote ya “operesheni maalum ya kijeshi” nchini humo kwa namna yoyote ile.
Pamoja na msimamo huo mkali, waziri huyo ameacha wazi mlango wa kidiplomasia. Amebainisha kuwa serikali ya Moscow iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu mzozo wa Ukraine endapo tu Serikali ya Marekani (Washington) itaonyesha utayari wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo.