WASHINGTON — Seneti ya Marekani imepitisha azimio linalojulikana kama “War Powers Resolution” linalolenga kupunguza mamlaka ya serikali kufanya hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Hatua hiyo imefikiwa baada ya majaribio manane ya kulipitisha azimio hilo.
Katika upigaji kura uliofanyika Senetini, azimio hilo liliidhinishwa kwa kura 50 za kuunga mkono dhidi ya 47 za kupinga. Maseneta wanne wa chama cha Republican walivunja msimamo wa chama chao na kuunga mkono azimio hilo. Wakati huohuo, Seneta wa chama cha Democratic John Fetterman alipiga kura ya kupinga hatua hiyo kinyume na msimamo wa chama chake.
Azimio hilo linatarajiwa kuendelea katika hatua za mwisho za mchakato wa kisheria ndani ya Seneti kabla ya kupelekwa katika Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kujadiliwa na kupigiwa kura.
Iwapo litapitishwa na mabunge yote mawili, kuna uwezekano Rais Donald Trump akatumia mamlaka yake ya kupinga muswada huo (veto), kutokana na msimamo wake wa awali kuhusu Iran. Ili kupindua veto ya rais, Seneti na Baraza la Wawakilishi zinahitaji kuunga mkono azimio hilo kwa theluthi mbili ya kura, jambo linaloonekana kuwa gumu kufikiwa katika mazingira ya sasa ya kisiasa nchini Marekani.