VIENNA, AUSTRIA — Katika tukio ambalo limezua hisia za kiusalama, Jeshi la Austria limelazimika kurusha ndege zake za kivita aina ya Eurofighter kwa siku mbili mfululizo, kufuatia ndege za Jeshi la Anga la Marekani (USAF) kugundulika zikiendesha shughuli zake ndani ya anga ya Austria bila kuwa na vibali halali vya kupita.
Hatua hii imechukuliwa kwa uzito mkubwa ikizingatiwa kuwa Austria ni taifa ambalo halifungamani na upande wowote kisiasa na kijeshi (neutral).
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, tukio la hivi karibuni lilishuhudiwa siku ya Jumapili ambapo ndege mbili za Marekani aina ya U-28A — ambazo ni toleo la PC-12 zinazotumiwa mahususi kwa oparesheni maalum za kijeshi — zilinaswa zikiruka juu ya eneo la milima ya Totes Gebirge, lililopo jimbo la Austria Juu.
Inaarifiwa kuwa, mara baada ya ndege hizo za Marekani kunaswa na kukabiliwa na ndege za kivita za Austria, zililazimika kugeuza mwelekeo mara moja na kurejea jijini Munich, nchini Ujerumani.
Msemaji wa Jeshi la Austria amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kupitia taarifa aliyoitoa kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter).
Serikali ya Austria imeongeza kuwa, masuala yote yanayoibuka kufuatia ukiukwaji huo wa anga yatashughulikiwa na kufuatiliwa zaidi kupitia njia rasmi za kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.