Uchambuzi wa picha za satelaiti uliofanywa na gazeti la Washington Post unaonyesha kuwa tangu kuanza kwa vita, mashambulizi ya Iran yameharibu au kuathiri angalau miundombinu na vifaa 228 katika vituo 15 vya kijeshi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo, malengo ya mashambulizi yalijumuisha hangari za ndege, mabweni ya wanajeshi, maghala ya mafuta, ndege, mifumo ya rada, vifaa vya mawasiliano, pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga kama Patriot na THAAD.
Ripoti inaonyesha kuwa Bahrain na Kuwait ndizo nchi zilizoathirika zaidi, huku pia athari zikiripotiwa katika Qatar, Saudi Arabia, Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kiwango cha uharibifu kilichobainishwa katika uchambuzi huu kinaelezwa kuwa kikubwa zaidi kuliko kile ambacho serikali ya Marekani imewahi kutangaza hadharani.
Taarifa zilizotolewa hapo awali zinaonyesha kuwa wanajeshi saba wa Marekani walipoteza maisha na zaidi ya 400 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.Wachambuzi wanasema picha za satelaiti zinaonyesha uharibifu uliotokea katika maeneo mbalimbali ya kijeshi na zinaibua maswali kuhusu uimara wa mifumo ya ulinzi katika eneo hilo.
Hadi sasa, Ikulu ya White House haijatoa tamko rasmi kuhusu matokeo ya uchambuzi huo.