Mfalme Mohammed VI wa Morocco amemteua Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mwanamfalme Moulay El Hassan (22), kushika wadhifa wa juu wa uratibu wa kijeshi ndani ya Vikosi vya Ulinzi vya Kifalme (FAR). Uteuzi huo unaashiria jukumu lake la kwanza la kiutendaji lenye uzito ndani ya jeshi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mwanamfalme amepewa nafasi ya “Mratibu wa Ofisi na Huduma za Makao Makuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Kifalme (FAR)”. Nafasi hiyo inachukuliwa kuwa muhimu kwa sababu inaunganisha shughuli za vifaa, ujasusi na mikakati ya kijeshi katika muundo wa juu wa uongozi wa jeshi.
Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanasema nafasi hiyo ni ya kiutendaji na inahusisha usimamizi wa karibu wa shughuli za jeshi, badala ya kuwa jukumu la heshima pekee.
Hatua hiyo pia inaonekana kufuata njia ile ile aliyopita Mfalme Mohammed VI alipokuwa mrithi wa kiti cha enzi, kabla ya kuchukua majukumu makubwa zaidi ya uongozi.