Washington – Mwanazuoni mashuhuri wa Marekani katika taaluma ya sayansi ya siasa na uhusiano wa kimataifa, Profesa John Mearsheimer, amesema kuwa Marekani ilishindwa kufikia malengo yake katika vita dhidi ya Iran, akieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa kosa kubwa la kimkakati.

Akizungumza kuhusu matokeo ya mzozo huo, Mearsheimer alisema kuwa Marekani iliingia vitani ikiwa na malengo manne makuu, lakini haikufanikiwa kuyatimiza.

Kwa mujibu wake, lengo la kwanza lilikuwa kuilazimisha Iran kuachana kabisa na uwezo wake wa kurutubisha nyuklia. Lengo la pili lilikuwa kuisimamisha kuunga mkono makundi kama Wahouthi (Ansarullah), Hamas na Hezbollah. Tatu, ilikuwa kuharibu au kuondoa kabisa makombora ya Iran. Na lengo la nne, ambalo alilitaja kuwa muhimu zaidi, lilikuwa kubadilisha utawala wa Iran.

Alifafanua kuwa mabadiliko ya utawala yalionekana kuwa msingi wa kufanikisha malengo mengine matatu, kwani kulingana na mantiki ya wakati huo, kubadilika kwa utawala kungesababisha pia mabadiliko ya sera za nyuklia, kijeshi na kikanda.

Hata hivyo, Mearsheimer alikiri kuwa hakuna hata lengo moja lililofikiwa. “Ukweli ni kwamba tulishindwa katika malengo yote manne, na kwa namna fulani tumeifanya hali kuwa mbaya zaidi,” alisema.

Kuhusu suala la makombora, alieleza kuwa somo kubwa ambalo Iran imejifunza kutokana na vita hivyo ni umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa makombora na majukwaa ya kurushia, pamoja na kuyaweka katika maeneo yaliyofichwa kama “miji ya makombora”.

Katika muktadha wa nyuklia, alionya kuwa hali ya sasa inaweza kuisukuma Iran zaidi kuelekea kutafuta silaha za nyuklia kwa mtazamo wa kujilinda.

Aidha, alibainisha kuwa hali ya kimkakati imebadilika katika Mlango-bahari wa Hormuz, akidai kuwa Iran sasa ina udhibiti mkubwa zaidi katika eneo hilo na imeanzisha kile alichokiita “kituo cha ukaguzi” — jambo ambalo hakuwapo kabla ya vita.Kwa mtazamo wake, ni vigumu kwa Iran kuachia udhibiti huo bila kupata manufaa makubwa katika makubaliano yoyote yajayo.

Akihitimisha, Mearsheimer alisisitiza kuwa vita hiyo ilikuwa kosa la wazi la kimkakati na mfano wa kushindwa kwa sera za nje za Marekani katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *