DAKAR, SENEGAL – Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko, ameyashutumu vikali mataifa ya Magharibi kwa kile alichokieleza kuwa ni jaribio la kulazimisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kiongozi huyo alitoa matamshi hayo alipokuwa akihutubia Bunge la Taifa siku ya Ijumaa. Katika hotuba yake, Bw. Sonko alitetea sheria mpya kali zinazolenga kudhibiti mapenzi ya jinsia moja nchini Senegal, hatua ambayo imeendelea kuvutia ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu.

“Kuna aina fulani ya ubabe unaofanywa. Kuna wanadamu bilioni nane duniani, lakini kuna kikundi kidogo kinachoitwa Magharibi ambacho, kwa sababu kina rasilimali na kinadhibiti vyombo vya habari, kinataka kuulazimisha ulimwengu uliosalia kukubali [ushoga],” alisema Sonko.

Sheria hiyo mpya, iliyoanza kutekelezwa rasmi mwishoni mwa mwezi Machi, imeongeza adhabu ya kifungo jela maradufu kwa wale watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, kutoka miaka mitano hadi miaka 10.

Vilevile, sheria hiyo inafanya kuwa kosa la jinai kitendo cha kufadhili mahusiano hayo, pamoja na kile kilichoelezwa kwenye sheria kama “kutukuza matendo yasiyo ya asili”, kipengele kinachojumuisha kuhamasisha au kujihusisha na vitendo hivyo.

Awali, Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Volker Turk, alimtaka Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, kutoidhinisha sheria hiyo, akiielezea kuwa inatia “wasiwasi mkubwa”.

“Sheria hii inawaweka watu katika hatari ya kufanyiwa uhalifu wa chuki, unyanyasaji, ukamataji holela, utapeli, na ubaguzi ulioenea katika sekta za elimu, afya, ajira na makazi,” alisema Turk wakati huo. Aliongeza kuwa sheria hiyo inazuia kazi halali za watetezi wa haki za binadamu, vyombo vya habari, na uhuru wa kujieleza kwa kila raia nchini Senegal.

Kupitishwa na kutekelezwa kwa sheria hii mpya kunakuja wakati kukiwa na ripoti za ongezeko la ukamataji wa watu wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *