Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, ametoa tamko zito akisisitiza kuwa ushiriki wa nchi hiyo katika mazungumzo ya kimataifa si ishara ya udhaifu wala kujisalimisha, bali ni hatua ya kulinda maslahi ya taifa kwa kutumia nguvu na heshima.

Akizungumza kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumatatu usiku, Rais Pezeshkian alibainisha kuwa Iran inaingia kwenye meza ya mazungumzo ikiwa na azma thabiti ya kulinda haki za wananchi wake bila kurudi nyuma.”Mazungumzo hayamaanishi kujisalimisha.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaingia kwenye mazungumzo kwa heshima na nguvu huku ikilinda haki za taifa, na kamwe haitarudi nyuma kutoka kwenye haki za kisheria za watu na nchi hii,” alisema Kiongozi huyo.

Rais aliongeza kuwa serikali yake itatumia mantiki na nguvu zote kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa, akisema: “Hata ikiwa ni kwa gharama ya maisha yetu, tutawatumikia wananchi na kulinda heshima ya Iran.”

Kauli hii ya Rais imekuja wakati ambapo Iran inaendelea na juhudi kubwa za kidiplomasia zenye lengo la kuhitimisha vita vilivyochochewa na Marekani pamoja na utawala wa Israel tangu tarehe 28 Februari.

Hadi sasa, Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa amani ya kudumu katika eneo hilo itategemea kuheshimiwa kwa mamlaka ya Iran na kukomeshwa kwa uvamizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *