Iraq na Pakistan zimeingia katika makubaliano maalum ya nishati na Iran kwa lengo la kuhakikisha usafirishaji salama wa mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) kupitia Mlango wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa ushawishi na udhibiti wa Iran katika eneo hilo muhimu la bahari.Iraq imeripotiwa kupata kibali cha usafirishaji salama kwa meli mbili kubwa za mafuta aina ya VLCC, zenye uwezo wa kubeba takribani mapipa milioni mbili kila moja, ili kulinda mapato yake ya taifa yanayotokana na mafuta.
Nayo Pakistan imefanikiwa kuhakikisha usafirishaji wa meli mbili za LNG kutoka Qatar kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka wakati wa msimu wa joto.Aidha, Iran imeanza kuweka utaratibu rasmi wa udhibiti wa usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz kwa kuhitaji nyaraka za kina za meli zote zinazopita pamoja na kusimamia safari hizo kupitia vikosi vyake vya majini.
Wakati huo huo, ripoti zinaonesha kuwa kiwango cha meli zinazopita katika eneo hilo kimeporomoka hadi asilimia tano pekee ya wastani wa kabla ya vita, ambapo takribani meli 3,000 zilikuwa zikivuka kila mwezi.Kupungua kwa shughuli hizo kumesababisha bei ya mafuta ghafi aina ya Brent kupanda kwa zaidi ya asilimia 50, huku bei za LNG zikiongezeka kati ya asilimia 35 hadi 50.
Nchi nyingine pia zinaelezwa kuanza kutafuta makubaliano yanayofanana na hayo ili kulinda usafirishaji wa nishati kupitia eneo hilo muhimu duniani.