Gazeti la New York Times, likiwanukuu maafisa wa Marekani, limeripoti kuwa taasisi za ujasusi za Marekani zina wasiwasi kwamba China inaweza kupata ufikiaji wa teknolojia nyeti zinazohusiana na ndege za kivita aina ya F-35 kupitia ushirikiano wa kijeshi na kiteknolojia kati ya Beijing na Riyadh.
Wasiwasi huo unatokana na uwezekano kwamba uhusiano wa karibu wa Saudi Arabia na China katika sekta za kijeshi na teknolojia unaweza kuongeza hatari ya taarifa au teknolojia zinazohusiana na F-35 kufikiwa na Beijing.
Aidha, moja ya ripoti za Shirika la Ujasusi wa Ulinzi la Marekani (DIA) imetaja uwezekano wa wanajeshi wa China kupata ufikiaji wa baadhi ya kambi za kijeshi nchini Saudi Arabia.
Ripoti hiyo pia imeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa teknolojia za China kutumika katika miundombinu ya mawasiliano ya Saudi Arabia, jambo ambalo maafisa wa Marekani wanaliona kuwa linaweza kuwa na athari za kiusalama iwapo mifumo hiyo itakuwa karibu au kuunganishwa na teknolojia nyeti za kijeshi za Marekani.
Chanzo: New York Times