Mahakama Nchini Afrika Kusini imeamuru Mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Bellarmine Mugabe, kufukuzwa Nchini humo baada ya kukiri kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na ukiukwaji wa taratibu za uhamiaji.
Katika hukumu hiyo, Mahakama imeeleza kuwa Mugabe mwenye umri wa miaka 28 atatakiwa kulipa faini ya dola za Kimarekani 36,000 sawa na takriban shilingi milioni 93.6 za Kitanzania na kuagiza kurejeshwa Zimbabwe mara moja baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa za kesi hiyo, Mugabe amekamatwa Februari 19, 2026 kufuatia tukio la kumpiga risasi Mlinzi wa Nyumbani kwake Mjini Johannesburg na kumjeruhi vibaya.