Jenerali wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), Gadi Eisenkot, ameibuka kuwa mpinzani mkuu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuelekea uchaguzi wa Oktoba 27, huku kura za maoni zikionyesha chama chake kipya, Yashar, kikiongoza kwa tofauti ndogo dhidi ya chama tawala cha Likud.

Kwa mujibu wa kura ya maoni ya Channel 12, asilimia 43 ya waliohojiwa wanamuunga mkono Eisenkot kuwa waziri mkuu, ikilinganishwa na asilimia 34 wanaomuunga mkono Netanyahu. Wakati huohuo, utafiti wa Channel 13 unaonyesha chama cha Yashar kinaweza kupata viti 23 kati ya 120 vya bunge, dhidi ya viti 22 vinavyotarajiwa kwa Likud.

Eisenkot mwenye umri wa miaka 66, ambaye alipoteza mwanawe na wapwa wake wawili katika vita vya Gaza, amesema kugombea kwake kunalenga kuleta mabadiliko na kulipa heshima kwa waliopoteza maisha katika mzozo huo. Historia yake ya kijeshi imempa uungwaji mkono mkubwa, ingawa pia amekosolewa kwa kuhusishwa na Dahiya Doctrine, mkakati wa kijeshi uliotumiwa katika operesheni za Gaza na Lebanon na uliopingwa na baadhi ya serikali za kigeni pamoja na mashirika ya haki za binadamu.

Katika kampeni zake, Eisenkot ameahidi kuiondoa serikali ya Netanyahu, akisema ana azma ya kuunda uongozi mpya. Hata hivyo, anakabiliwa na changamoto za kisiasa, ikiwemo kujenga muungano wa kutawala, msimamo wake wa kutaka huduma ya kijeshi kwa wote, na kupinga ushiriki wa baadhi ya wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia serikalini.

Ingawa anapinga kuundwa kwa taifa la Palestina, Eisenkot amesema yuko tayari kushirikiana na vyama vya Waarabu iwapo vitakubali mfumo wa huduma ya kitaifa usio wa kijeshi. Wachambuzi wanaonya kuwa umaarufu wake wa sasa utapimwa na uwezo wake wa kufanya maridhiano ya kisiasa katika kipindi cha kampeni.

Chanzo: Bloomberg

Leave a Reply