Kiongozi Mkuu wa Iran ametoa tamko zito akiahidi kuwa nchi hiyo itachukua hatua kali za kulipiza kisasi dhidi ya wauaji wa aliyekuwa kiongozi wao, akisisitiza kuwa operesheni hiyo itashirikisha watu wenye msimamo huru duniani kote hivi karibuni.
Katika hotuba yake iliyolenga kuonyesha msimamo usiotikisika wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu, Kiongozi huyo amebainisha kuwa kisasi hicho si cha hiari bali ni takwa la wananchi. Amesema kuwa mpango huo wa kulipiza kisasi hautegemei uwepo wake au viongozi wengine madarakani, bali ni ahadi ambayo “lazima itimie.”
“Wauaji wa kiongozi aliyetangulia lazima wajue kuwa watawajibishwa kwa jinai zao,” alionya Kiongozi huyo, akiongeza kuwa damu ya mashahidi haiwezi kupotea bure na ni wajibu wa kitaifa kuhakikisha haki inatendeka.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza umakini wa kiusalama katika ukanda huo, huku Iran ikionekana kuandaa mazingira ya kimataifa kutekeleza kile inachokiita “haki kwa mashahidi wake.”