WASHINGTON D.C. — Jeshi la Marekani limejipata katika hali isiyo ya kawaida baada ya kukubali kupokea ndege za kivita aina ya F-35B Joint Strike Fighters zisizo na rada, uamuzi unaochochewa na changamoto kubwa za uzalishaji wa vifaa vya teknolojia ya juu.
Kwa mujibu wa ripoti ya TWZ, jeshi hilo limepokea takriban ndege sita za aina hiyo kwa ajili ya Jeshi la Majini la Marekani (U.S. Marine Corps). Ndege hizi hazina rada muhimu ya AN/APG-85, ambayo inatarajiwa kuanza kutengenezwa rasmi ifikapo Aprili 2028.
Akizungumzia hali hiyo, Gregory Masiello, ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Pamoja ya Mpango wa F-35, amekiri hadharani kuwa ndege hizo haziwezi kutumika kikamilifu katika operesheni za kijeshi bila mfumo huo wa rada.
Changamoto ya ‘Block 4’ na Kushuka kwa Uwezo
Tatizo hili la rada ni sehemu ya changamoto pana inayolikabili jeshi hilo kuhusiana na maboresho ya mfumo wa Block 4. Hali hii inakuja wakati ripoti mpya ya serikali ikitoa takwimu za kusikitisha kuhusu utayari wa ndege hizo.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kati ya mwaka wa fedha wa 2020 na 2025, uwezo wa jumla wa ndege zote za F-35 kutekeleza majukumu yao (Full Mission Capable rate) umeporomoka kwa kiasi kikubwa, kutoka asilimia 38 hadi asilimia 25 pekee.
Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanaeleza kuwa ucheleweshaji huu wa vifaa ni pigo kwa utayari wa anga wa Marekani, huku kukiwa na shinikizo la kuendeleza teknolojia hiyo tata ya ndege za kivita.