PARIS, UFARANSA
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ametoa msimamo thabiti na wa tahadhari kuhusiana na mzozo wa Iran, akisisitiza kuwa mabadiliko ya utawala nchini humo hayawezi na hayapaswi kupatikana kupitia mashambulizi ya kijeshi au mabomu.
Akizungumzia shinikizo la kisiasa lililokuwepo huko nyuma, Rais Macron alibainisha kuwa alishuhudia uwepo wa watu ndani ya serikali ya aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na washirika wa kikanda, waliokuwa wakihimiza hatua kali na za mbali zaidi dhidi ya Tehran.
Kwa mujibu wa Macron, mabadiliko ya mfumo wa uongozi katika nchi yoyote ni jukumu ambalo kimsingi linapaswa kutekelezwa na wananchi wenyewe wa nchi husika. Aliongeza kuwa jaribio lolote la nje la kulazimisha mabadiliko hayo linahitaji operesheni kubwa za kijeshi za ardhini na vita vya muda mrefu vinavyoweza kudumu kwa miaka mingi.
Akitoa mfano hai wa kushindwa kwa mikakati hiyo, Kiongozi huyo wa Ufaransa aliikumbusha dunia kuhusu hali iliyotokea nchini Afghanistan.
“Angalieni kilichotokea Afghanistan. Je, mabadiliko ya utawala yalifanikiwa baada ya zaidi ya miaka kumi ya vita? Jibu ni hapana,” alisema Macron.
Rais Macron alihitimisha kwa kutoa wito kwa viongozi wa kimataifa kuwa na kiasi, unyenyekevu, na mtazamo wa wazi (lucidity) katika kushughulikia mizozo ya kidiplomasia, akionya kuwa nguvu ya kijeshi pekee si suluhu ya kudumu ya mabadiliko ya kisiasa.