WASHINGTON D.C. — Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu mahusiano yake ya kidiplomasia na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akimtaja kiongozi huyo kuwa amekuwa na “shauku iliyopitiliza” katika mambo makuu mawili tangu mwaka 2009.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Clinton amefichua kuwa tangu alipoanza kufanya kazi na Netanyahu, vipaumbele vya kiongozi huyo vimekuwa ni kuishambulia kijeshi Iran na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya Saudi Arabia.
Clinton alikumbushia mkutano wake wa kwanza rasmi na Netanyahu mwaka 2009, ambapo ajenda kuu ya kiongozi huyo wa Israel ilikuwa ni kutaka kujua namna Marekani inavyoweza kusaidia katika kuishinda na “kuisambaratisha kabisa” Iran (decapitation), huku akitaka njia za mkato za kuleta maridhiano na Saudi Arabia.
Shinikizo lisilokoma la kijeshi
Clinton ameeleza kuwa wakati wa uongozi wake katika wizara ya mambo ya nje, Netanyahu na serikali yake walikuwa wakitoa shinikizo lisilokoma kwa Marekani ili iunge mkono mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
“Lilikuwa ni shinikizo la kila wakati, lisilopungua hata kidogo,” alisema Clinton.
Aliongeza kuwa maafisa wa Israel walikuwa wakitumia lugha ya dharura kujaribu kuishawishi Marekani, wakisema: “Ndege zetu tayari zipo kwenye njia ya kurukia (tarmac),” wakimaanisha kuwa walikuwa tayari kurusha makombora wakati wowote.
Hata hivyo, Clinton alifichua kuwa jibu lake kwa viongozi hao lilikuwa fupi na la kejeli kidogo: “Haya, kila la heri.”
Kuchezewa shere na mshirika
Sehemu nyingine ya kuvutia katika ufafanuzi huo ni pale Clinton alipoulizwa iwapo alihisi Marekani “inachezewa shere” au kutumiwa na mshirika wake huyo (Israel), ambaye anapokea mabilioni ya dola kama msaada wa kijeshi na kiuchumi kutoka Washington.
Bila kusita, Clinton alijibu: “Kila wakati.”
Kauli hizi za Clinton zinatoa taswira mpya ya kile kinachoonekana kuwa ni mvutano wa siri uliokuwepo nyuma ya pazia kati ya utawala wa Marekani na serikali ya Netanyahu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, hasa kuhusiana na usalama wa Mashariki ya Kati.