BEIJING, China – Serikali ya China kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, imethibitisha rasmi kumkamata na kumzuilia raia mmoja wa Marekani, hatua inayozua sura mpya ya mvutano kati ya mataifa hayo mawili makubwa duniani.
Raia huyo aliyetambulika kwa jina la U Min Zin, anashikiliwa na mamlaka za usalama nchini humo kwa tuhuma nzito za kuhusika na vitendo vya ujasusi.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo, China imebainisha kuwa U Min Zin anachunguzwa kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa wa Jamhuri ya Watu wa China. Ingawa maelezo zaidi juu ya mazingira ya ukamataji wake hayakuwekwa wazi mara moja, mamlaka zimesisitiza kuwa hatua hiyo imezingatia sheria za nchi hiyo kuhusu ulinzi na usalama.