DAR ES SALAAM — Tume Maalumu iliyoundwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali, imesema uchunguzi wake umewakuta masheikh watatu na makosa yanayohusiana na maadili na uongozi.

Akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo, Katibu wake, Dkt. Abdallah Tego, amesema uchunguzi ulihusisha aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar Kawambwa; Sheikh wa Mkoa wa Singida, Sheikh Issa Nassor Issa; na Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Sheikh Hassan Idi Kiburwa.

Kwa mujibu wa Tume, katika mchakato wa uchunguzi ilikusanya na kupitia nyaraka mbalimbali pamoja na taarifa zilizochapishwa mitandaoni. Pia ilifanya mahojiano ya ana kwa ana na kwa simu na mashahidi, wakiwemo viongozi waliowahi kufanya kazi kwa karibu na masheikh hao.

Tume imesema Sheikh Issa Nassor Issa na Sheikh Hassan Idi Kiburwa waliitikia wito na kufika kutoa maelezo yao. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utetezi wao ulisaidia kupunguza uzito wa baadhi ya makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

Hata hivyo, Tume imesema Sheikh Walid Alhad Omar Kawambwa hakufika mbele yake kutoa utetezi licha ya juhudi zilizofanywa kumtafuta.

Uamuzi wa Mwisho Kusubiri Baraza la Ulamaa

Tume imewasihi masheikh hao kuheshimu uamuzi utakaotolewa na Baraza la Ulamaa, ikisema hatua zinazochukuliwa zinalenga kulinda maslahi ya umma wa Kiislamu.

Pia imewataka Waislamu na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu wakati wakisubiri uamuzi wa mwisho wa Baraza la Ulamaa.

Maoni