Rais Donald Trump amemshambulia Waziri Mkuu wa Ontario, Doug Ford, na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, akidai kuwa Canada imekuwa ikinufaika na Marekani kwa miongo kadhaa na sasa haitaruhusiwa tena kufanya hivyo.

Katika ujumbe wake, Trump alimuelezea Ford kwa maneno makali, akisema ni

“ndugu asiye na mvuto, akili na uwezo wa kisiasa” wa aliyekuwa meya wa Toronto, Rob Ford.

Trump amesema:

“Marekani imekuwa ikiibeba Canada kwa miongo kadhaa, lakini hilo limekwisha.”

Amedai kuwa Marekani ni kubwa zaidi kiuchumi na kijeshi kuliko Canada, na kuongeza kuwa bila msaada wa Marekani, Canada “isingeweza kuendelea.”

Trump pia alidai kuwa Canada inategemea Marekani katika usafirishaji wa nishati, akitaja umeme, mafuta na gesi vinavyopita kupitia miundombinu ya Marekani.
Ameonya kuwa ikiwa viongozi wa Canada hawatabadilisha msimamo wao kuhusu sera za biashara, nchi hiyo inaweza kukabiliwa na “matokeo mabaya zaidi.”

Kauli hiyo imekuja wakati uhusiano wa kibiashara kati ya Washington na Ottawa ukiwa na mvutano mkubwa kutokana na sera mpya za ushuru za Marekani.

Serikali ya Canada imepinga hatua hizo, huku viongozi wake wakisema watachukua hatua za kulinda maslahi ya taifa na kujibu ushuru wa Marekani kwa kiwango sawa.

Doug Ford, ambaye anaongoza jimbo la Ontario — eneo lenye uchumi mkubwa zaidi Canada — amekuwa mkosoaji wa baadhi ya sera za Trump, hasa kuhusu biashara na ushuru.

Leave a Reply