TEL AVIV, ISRAEL – Moshe Ya’alon, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa utawala wa Israel, ametoa kauli nzito ya kukiri kuwa mashambulizi ya kijeshi yaliyoelekezwa dhidi ya Iran hayakufikia malengo yoyote yaliyokusudiwa, hatua ambayo imeiweka Tel Aviv katika mazingira magumu ya kidiplomasia.

Katika tathmini yake ya wazi, Ya’alon amebainisha kuwa operesheni hizo zililenga kutimiza malengo makuu matatu: kuiangusha serikali ya Iran, kusambaratisha mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, na kudhoofisha uwezo wake wa makombora. Hata hivyo, amekiri kuwa hakuna hata lengo moja kati ya hayo lililoweza kufikiwa.

Kiongozi huyo wa zamani ameeleza kusikitishwa kwake na hali ya sasa, akibainisha kuwa washirika wao wa kimataifa, hususan Marekani, sasa wanaichukulia Israel kama mhusika mkuu wa kushindwa kwa operesheni hiyo.

“Nafikiri tumejiingiza wenyewe katika matatizo, na jambo baya zaidi ni kwamba Marekani inatulaumu sisi,” alinukuliwa Ya’alon.

Kauli hii ya Ya’alon imezua mjadala mpana ndani na nje ya Israel kuhusu ufanisi wa mikakati yao ya kijeshi katika ukanda huu, na inaonekana kama dhoruba ya kisiasa inayozidi kuweka wazi nyufa za kimkakati katika utawala wa Tel Aviv.

Leave a Reply