Uganda imemuidhinisha mwanadiplomasia na mwanasiasa mkongwe Olara Otunnu kuwa mgombea wake katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa (UN).

Otunnu, ambaye anaungwa mkono na serikali ya Uganda, yuko mjini New York kwa ajili ya kukutana na ujumbe wa nchi wanachama na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Baraza la Usalama la UN, kwa mujibu wa Balozi wa Kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, Adonia Ayebare.

Ayebare amesema safari hiyo inalenga kumpa Otunnu fursa ya kuwasilisha maono yake na kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja na wadau muhimu katika mchakato wa kumpata kiongozi mpya wa Umoja wa Mataifa.

Olara Otunnu ana uzoefu mkubwa katika diplomasia ya kimataifa. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Oxford na Shule ya Sheria ya Harvard (Harvard Law School), kabla ya kuanza kazi yake katika masuala ya kimataifa.

Kati ya mwaka 1980 na 1985, Otunnu aliwahi kuwa mwakilishi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, ambapo alihudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja kama Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Pia aliwahi kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Watoto na Migogoro ya Kivita kati ya mwaka 1997 na 2005, akiongoza juhudi za kimataifa za kulinda watoto katika maeneo yenye vita.

Katika kinyang’anyiro hicho, Otunnu anatarajiwa kutumia uzoefu wake wa muda mrefu katika diplomasia, usuluhishi wa migogoro na masuala ya amani ili kujenga uungwaji mkono kutoka mataifa mbalimbali.

Leave a Reply