Kundi linaloitwa Jukwaa la Msaada wa Kielektroniki (Cyber Support Front) limedai kufanya shambulio kubwa la kimtandao dhidi ya taasisi za kifedha za Israel, likisema limeharibu takribani terabaiti 120 za taarifa nyeti za kifedha na kiulinzi za taifa hilo.

Katika taarifa iliyotolewa, kundi hilo lilidai kuwa lilifanikiwa kuvamia mifumo ya taasisi kadhaa muhimu za kifedha na uhasibu, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya kiuchumi na mifumo ya kodi ya Israel.

Limetaja kampuni tatu za kifedha kuwa zililengwa katika operesheni hiyo, ikiwemo kampuni ya uhasibu na ukaguzi ya Oren Levy, kampuni ya ushauri wa kifedha na kodi ya Finco pamoja na kampuni ya Milkovsky Consulting and Investment iliyopo Tel Aviv.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kundi hilo lilidai kufuta takribani terabaiti 120 za data pamoja na nakala zake za kuhifadhi taarifa (backup), hatua ambayo lilisema ilisababisha mifumo ya kompyuta, seva za kuhifadhi data na miundombinu ya mawasiliano ya taasisi hizo kushindwa kufanya kazi.

Kundi hilo pia lilidai kuwa shambulio hilo limesababisha usumbufu katika shughuli za kifedha na kodi, huku wateja wa kampuni hizo wakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma.

Leave a Reply