Macron kuzuru Nigeria katika hatua mpya ya kuimarisha uhusiano wa kimkakati na Abuja
Ufaransa na Nigeria zinaelekea kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, huku Rais Emmanuel Macron akitarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Nigeria baadaye mwaka huu, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kuimarisha ushawishi na uhusiano wa mataifa hayo mawili katika kipindi cha ushindani mkubwa wa kimataifa.
Balozi wa Ufaransa nchini Nigeria, Marc Fonbaustier, ametangaza kuwa Rais Macron atafanya ziara hiyo ya kitaifa nchini humo, ikiwa ni miaka miwili baada ya Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, kufanya ziara rasmi mjini Paris.
Tangazo hilo lilitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Ufaransa yaliyofanyika jijini Abuja, likiwa limeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara, usalama, kilimo, utamaduni na maendeleo ya kikanda.
Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali ya Nigeria, wabunge, wanadiplomasia na wafanyabiashara, Balozi Fonbaustier alisema ziara ya Macron itatoa nafasi kwa viongozi hao wawili kupitia maendeleo yaliyopatikana katika mpango wa pamoja wa ushirikiano na kuweka mikakati mipya ya uhusiano wa muda mrefu.
“Nina furaha na heshima kutangaza kwamba, miaka miwili baada ya ziara ya Rais Bola Ahmed Tinubu mjini Paris, Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Emmanuel Macron, atasafiri kwenda Nigeria kwa ziara nyingine rasmi ya kitaifa msimu huu wa vuli,” alisema balozi huyo.
Aliongeza kuwa viongozi hao wataangalia mafanikio ya mpango wa pamoja wa ushirikiano na kubainisha maeneo muhimu yatakayounda uhusiano wao katika miaka ijayo.
“Kwa pamoja, marais wetu watatathmini maendeleo ya mpango wetu na kuweka mambo muhimu yatakayojenga uhusiano wetu kwa siku zijazo. Haya yatakuwa na malengo makubwa na manufaa kwa wananchi wa mataifa yetu mawili,” alisema.
Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Nigeria, ambayo ni uchumi mkubwa zaidi Afrika, na Ufaransa, moja ya mataifa yenye nguvu kiuchumi na kisiasa barani Ulaya.
Hatua hiyo inakuja wakati mataifa mbalimbali duniani yakiongeza juhudi za kujenga ushirikiano mpya wa kiuchumi na kimkakati barani Afrika, hasa katika sekta za nishati, teknolojia, biashara na usalama.
Balozi Fonbaustier alielezea uhusiano wa Nigeria na Ufaransa kama “ushirikiano wa nchi zilizo sawa,” akisisitiza kuwa mahusiano hayo yanajengwa juu ya kuheshimiana na si kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Alisema mataifa hayo yana malengo yanayofanana katika kukuza uchumi, kuongeza nafasi za ajira, kulinda mazingira na kuimarisha amani katika eneo la Afrika Magharibi.
Pia alisisitiza kuwa Nigeria na Ufaransa zinaendelea kushirikiana katika kutetea misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, huku zikilenga kujenga mazingira ya amani na maendeleo kwa wananchi wao.
Ziara ya Macron sasa inatarajiwa kuwa fursa ya viongozi hao kuweka mikakati mipya ya ushirikiano, huku ikionyesha nafasi inayoongezeka ya Nigeria katika diplomasia ya kimataifa na uhusiano wa Afrika na mataifa ya Magharibi.