Kombora la Sejjil la Iran likirushwaPicha: Wikimedia Commons / Fars Media Corporation, CC BY 4.0

Jeshi la Iran limetangaza mpango wa kuboresha uwezo wa makombora yake kwa kuongeza umbali na kasi, likisema mabadiliko ya namna Marekani inavyoendesha operesheni zake yamelazimisha Tehran kurekebisha mkakati wake wa kijeshi.

Msemaji wa Jeshi la Iran, Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia, amesema uzoefu wa vita vya hivi karibuni umeonyesha haja ya kuongeza uwezo wa kufikia malengo yaliyo mbali zaidi.

Kwa mujibu wa maelezo yake, vikosi vya Marekani sasa vinafanya baadhi ya operesheni zake vikiwa hadi kilomita 1,000 kutoka pwani ya Iran, hali inayopunguza ufanisi wa baadhi ya mifumo ya sasa ya makombora ya Tehran.

Akraminia amesema makombora yaliyotumiwa dhidi ya vituo vya kijeshi na meli wakati wa mapigano yalifanya vizuri, lakini tathmini ya kijeshi imeonyesha kuwa Iran inahitaji kuongeza uwezo wake wa mashambulizi ya masafa marefu.

Mpango huo unaweza kuongeza mvutano katika Ghuba, hasa wakati Washington na Tehran zikiendelea kuwasiliana kupitia wapatanishi kuhusu Mlango wa Hormuz na uwezekano wa kuzuia kurejea kwa vita vikubwa.

Vyanzo: The Cradle, Asharq Al-Awsat.

Maoni