MOSCOW, RUSSIA – Iran na Russia zimepiga hatua kubwa katika kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi na kiufundi, huku zikiongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya nishati ya nyuklia na ujenzi wa njia mpya ya kimkakati ya usafirishaji bidhaa.
Katika kongamano la kisayansi lililofanyika jijini Moscow kuhusu ushirikiano wa mataifa hayo mawili, Balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali, ametangaza kuwa mataifa hayo yamesaini mkataba wa maelewano (MoU) wenye thamani ya dola bilioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nguvu ya nyuklia katika mkoa wa Hormozgan, nchini Iran.
Balozi Jalali amesisitiza kuwa mradi wa ‘International North-South Transport Corridor’ (INSTC) umekuwa nguzo muhimu kwa uchumi wa nchi hizo mbili. Njia hii ya usafirishaji, inayounganisha Russia na kaskazini mwa Ulaya na Bahari ya Hindi kupitia Iran, imetajwa kuwa muhimu zaidi kutokana na changamoto za kiusalama zinazozikabili njia za bahari duniani kwa sasa.
“Tawi la mashariki la njia hii tayari linapitisha zaidi ya tani milioni 3 za bidhaa, huku likiwa na uwezo wa kuhimili hadi tani milioni 15,” alisema Jalali.
Aidha, alibainisha kuwa mradi wa reli wa Rasht-Astara, wenye urefu wa kilomita 162, ndio kiungo muhimu kilichosalia ili kukamilisha njia hiyo ya magharibi. Kufuatia mazungumzo na Naibu Waziri wa Uchukuzi wa Russia, Jalali alithibitisha kuwa masuala ya ardhi kwa ajili ya reli hiyo yameshamalizika na mradi huo utakabidhiwa kwa Russia kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Katika sekta ya nishati ya nyuklia, ushirikiano kati ya Tehran na Moscow unaendelea kushika kasi. Mbali na mtambo wa Bushehr ambao tayari unafanya kazi na unaendelea kupanuliwa, mradi wa Hormozgan unatajwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa aina yake kuwahi kufanywa na sekta binafsi ya Iran kwa kushirikiana na kampuni ya Rosatom ya Russia.