Chanzo kimoja chenye taarifa kimesema kuwa Iran haitashiriki duru ya pili ya mazungumzo na Marekani hadi pale masharti matano ya kujenga imani yatakapotekelezwa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, masharti hayo yanahusisha kusitishwa kwa vita katika maeneo yote hususan Lebanon, kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran, kuachiliwa kwa fedha za Iran zilizozuiwa nje ya nchi, kulipwa fidia kwa madhara yaliyotokana na vita pamoja na kutambuliwa kwa mamlaka ya Iran katika Mlango wa Hormuz.

Chanzo hicho pia kilieleza kuwa Iran imeifikishia Pakistan, inayoshiriki kama mpatanishi, wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mzingiro wa baharini katika Bahari ya Arabia na Ghuba ya Oman hata baada ya kusitishwa kwa mapigano. Tehran inaona hali hiyo kuwa ishara ya kutokuaminika kwa mazungumzo na Marekani.

Iran imefafanua kuwa masharti hayo yana lengo la kujenga kiwango cha chini cha uaminifu kabla ya kurejea mezani kwa mazungumzo mapya. Viongozi wa Tehran wanaamini kuwa bila hatua za vitendo katika masuala hayo, mazungumzo mapya hayawezi kuanza.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa masharti hayo yalitolewa kama jibu kwa pendekezo la vipengele 14 kutoka Marekani, ambalo vyanzo vya Iran vinadai lilikuwa la upande mmoja na lililolenga zaidi maslahi ya Washington.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Marekani ilikuwa ikijaribu kupitia mazungumzo kufanikisha baadhi ya malengo ambayo haikuweza kuyapata kupitia vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *