Marekani inaripotiwa kushinikiza kurejeshwa kwa usafirishaji wa gesi asilia kutoka Urusi kwenda Ulaya kupitia Ukraine, kama sehemu ya juhudi za kufikia makubaliano ya kupunguza mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wall Street Journal iliyonukuliwa na Clash Report, wajumbe wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner, waliwasilisha pendekezo hilo wakati wa ziara zao Moscow na Kyiv mwezi Septemba.
Mpango huo unapendekeza gesi ya Urusi isafirishwe kupitia mtandao wa mabomba unaopita Ukraine, huku kampuni au taasisi ya Marekani ikitumika kama mpatanishi wa biashara hiyo.
Washington inaamini kuwa mpango huo unaweza kuisaidia Ukraine kupata mapato ya usafirishaji wa gesi na wakati huohuo kuishawishi Urusi kukubali makubaliano kuhusu usalama wa miundombinu ya nishati.
Hata hivyo, baadhi ya serikali za Ulaya zimepinga pendekezo hilo kwa kuhofia kurejea katika utegemezi wa nishati kutoka Urusi.
Ukraine ilisimamisha usafirishaji wa gesi ya Urusi kupitia ardhi yake Januari 2025 baada ya mkataba wake na kampuni ya Gazprom kumalizika.
Mpaka sasa, hakuna makubaliano rasmi yaliyotangazwa kati ya Marekani, Urusi, Ukraine na Umoja wa Ulaya kuhusu kurejesha usafirishaji huo.

Maoni