DODOMA — Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imeagiza shule zote za awali, msingi na sekondari Tanzania Bara kufungwa Novemba 13, 2026, badala ya Desemba 4 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Na. 3 wa Mwaka 2026 uliotolewa Septemba 30, uamuzi huo umechukuliwa kufuatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa mvua kubwa zinazohusishwa na El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.
Wizara imesema mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko na athari nyingine katika baadhi ya maeneo na kuathiri shughuli za uendeshaji wa shule. Hatua hiyo inalenga kulinda usalama na ustawi wa wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule.
Mabadiliko hayo yanarekebisha kalenda iliyowekwa kupitia Waraka wa Elimu Na. 6 wa Mwaka 2025 kwa shule za awali, msingi na sekondari pamoja na Waraka Na. 1 wa Mwaka 2026 kwa Kidato cha Tano na Sita, ambazo zilielekeza shule kufungwa Desemba 4.
Waraka mpya, uliosainiwa na Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa, umeanza kutumika rasmi Oktoba 1, 2026.
Chanzo: Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia — Waraka wa Elimu Na. 3 wa Mwaka 2026.