Taarifa zinazozunguka kwenye masoko ya nishati zinaonyesha kuwa akiba ya mafuta ghafi ya Marekani imefikia kiwango cha chini kinachoweza kuhudumia mahitaji ya nchi hiyo kwa takriban siku 41 pekee, kiwango kinachodaiwa kuwa cha chini zaidi katika kipindi cha karibu nusu karne.
Hali hiyo imeongeza wasiwasi kuhusu uwezo wa Marekani kukabiliana na mishtuko ya usambazaji wa mafuta, hasa wakati kukiwa na mvutano wa kisiasa na kijeshi katika maeneo muhimu ya uzalishaji wa nishati duniani.
Akiba ya mafuta ya kimkakati ya Marekani (Strategic Petroleum Reserve – SPR) imekuwa ikitumika kama kinga ya dharura pale kunapotokea changamoto kubwa kwenye soko la mafuta, kama vita, vikwazo au kukatika kwa usafirishaji.
Kupungua kwa akiba hiyo kunakuja wakati masoko ya nishati yakikabiliwa na shinikizo kutokana na migogoro ya kimataifa, ikiwemo mvutano katika Mashariki ya Kati na wasiwasi kuhusu usalama wa njia muhimu za usafirishaji wa mafuta.