Trump atoa onyo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ataja Bahari ya Hormuz kuwa eneo la Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ametoa onyo kali kuhusu suala la nyuklia la Iran, akisema Washington haitaruhusu Tehran kupata silaha ya nyuklia.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Myrtle Beach, jimbo la South Carolina, Trump alisema kuwa Iran haipaswi kumiliki silaha hiyo na kuonya kwamba hatua kubwa zinaweza kuchukuliwa iwapo hilo litatokea.

“Hatuwezi kuwaruhusu wawe na silaha ya nyuklia, hatuwezi kuiruhusu Iran iwe na silaha ya nyuklia, la sivyo mtayaona mambo mabaya sana,” alisema Trump.

Katika hotuba hiyo, Trump pia aliitaja Bahari ya Hormuz kama eneo la Marekani, kauli inayokuja katika kipindi ambacho njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani imekuwa kitovu cha mvutano wa kimataifa.

Bahari ya Hormuz ni njia muhimu inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, ambapo sehemu kubwa ya mafuta ya Mashariki ya Kati husafirishwa kwenda masoko ya dunia.

Kauli ya Trump imeongeza mjadala kuhusu msimamo wa Marekani dhidi ya Iran, huku suala la mpango wa nyuklia wa Tehran likiendelea kuwa moja ya masuala yenye mvutano mkubwa katika siasa za kimataifa.

Leave a Reply