Marekani imethibitisha kuwa wanajeshi wake wawili wameuawa nchini Jordan na mwingine bado hajulikani alipo, kufuatia mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (drones) yanayodaiwa kufanywa na Iran.
Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imetoa taarifa rasmi ikieleza kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mashambulizi yaliyolenga maeneo ya kijeshi nchini Jordan.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi wawili wa Marekani walifariki katika shambulio hilo, huku mwanajeshi mwingine akiendelea kutafutwa.
CENTCOM imesema wanajeshi wanne waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini nchini Jordan kwa matibabu na baadaye kuruhusiwa, huku wale waliopata majeraha madogo wakirejea kwenye majukumu yao.
Aidha, jeshi hilo limesema majina ya wanajeshi waliofariki hayatatangazwa mara moja, na yataendelea kuwa siri kwa muda wa saa 24 baada ya familia zao kufahamishwa rasmi, kwa mujibu wa taratibu za kijeshi za Marekani.
Tukio hilo linaongeza mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, huku Marekani na Iran zikiendelea kuwa katika mzozo unaohusisha mashambulizi na majibu ya kijeshi.