Serikali ya Oman imesema chanzo kikuu cha tishio kwa usalama na utulivu wa Mashariki ya Kati hakitokani na Iran, bali kinatokana na sera na hatua za Israel, huku ikitoa wito wa kuimarishwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia ili kumaliza migogoro inayoendelea katika eneo hilo.

Akizungumza kuhusu hali ya usalama katika Ghuba ya Uajemi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Al-Busaidi, alisema maamuzi yanayochukuliwa na Tel Aviv ndiyo yanayochochea kuongezeka kwa mvutano, na kusisitiza kuwa vita haviwezi kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za eneo hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr likinukuu Al Jazeera, Al-Busaidi alisema mazungumzo nyeti yanaendelea kwa lengo la kuweka mfumo wa muda mrefu utakaohakikisha usalama na uhuru wa usafiri wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Aliongeza kuwa Oman itaendelea kushirikiana na Iran pamoja na jamii ya kimataifa ili kufanikisha utaratibu utakaolinda usafiri wa meli na kudumisha utulivu katika njia hiyo muhimu ya kimataifa.

Waziri huyo alisisitiza kuwa tishio kubwa kwa usalama wa Ghuba ya Uajemi halitokani na nchi za eneo hilo, bali linachochewa na hatua zinazofanywa kutoka nje ya eneo, hususan Tel Aviv.

Aidha, alisema vita vinavyoendelea vimesababisha maafa makubwa ya kibinadamu, havikuidhinishwa na Umoja wa Mataifa, na hadi sasa havijafanikisha malengo yaliyokuwa yakidaiwa.

Wakati huo huo, mtandao wa Al Mayadeen uliripoti kuwa Al-Busaidi, katika makala aliyoiandika kwenye gazeti la Le Monde, alisisitiza kuwa changamoto kubwa ya usalama katika Mashariki ya Kati haitokani na Tehran bali na Tel Aviv.

Alitoa wito kwa mataifa ya eneo hilo na jumuiya ya kimataifa kujifunza kutokana na hali ya sasa na kuelekeza juhudi katika kujenga amani ya kudumu badala ya kuendeleza migogoro.

Leave a Reply