Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limewasilisha rasmi muswada wa sheria unaolenga kuimarisha usimamizi na ulinzi wa Mlango Bahari wa Hormuz, hatua inayokuja wakati mvutano ukiongezeka kufuatia kile Tehran inachokitaja kuwa ni uingiliaji wa kijeshi wa Marekani katika njia hiyo muhimu ya kimkakati.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran, Ebrahim Azizi, alitangaza hatua hiyo kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne. Alisema muswada huo umewasilishwa wakati vikosi vya Iran vikidai kutungua ndege zisizo na rubani za Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

“Usiku uliopita, sambamba na kuangamizwa kwa ndege zisizo na rubani za Marekani, mpango wa kimkakati wa kuhakikisha usalama na maendeleo endelevu ya Mlango Bahari wa Hormuz na Ghuba ya Uajemi ulitangazwa na kupokelewa rasmi katika kikao cha wazi cha Bunge,” alisema Azizi.

Alisisitiza kuwa Iran itaendelea kulinda kile ilichokiita mipaka yake isiyoweza kuvukwa, akibainisha kuwa usimamizi wa Mlango Bahari wa Hormuz ni sehemu ya maslahi ya msingi ya taifa hilo.

“Hii ni hatua ya kwanza; hatua nyingine zinafuata,” alisema, akidokeza kuwa Tehran inaweza kutangaza hatua zaidi katika siku zijazo ili kuimarisha usalama wa bahari na kulinda maslahi yake katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Mlango Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ya kimataifa inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa duniani, hivyo mabadiliko yoyote ya kiusalama katika eneo hilo huathiri moja kwa moja soko la nishati duniani.

Iran imeendelea kuweka vikwazo katika usafiri wa baadhi ya meli kupitia mlango huo tangu kuanza kwa vita ilivyovitaja kuwa vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani kwa kushirikiana na Israel mnamo Februari 28. Mapigano hayo yalisitishwa mwanzoni mwa Aprili baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Baadaye, mnamo Juni 17, Iran na Marekani zilisaini Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosimamiwa na Pakistan. Kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha makubaliano hayo, jukumu la kufungua tena na kusimamia usafiri katika Mlango Bahari wa Hormuz lilikabidhiwa rasmi kwa Iran.

Leave a Reply