Vita vinavyoendelea katika eneo la Donbass vimeingia katika hatua nyeti na ya maamuzi. Taarifa kutoka uwanja wa vita zinaonyesha kuwa vikosi vya Urusi vimefanikiwa kusonga mbele na sasa viko umbali wa takriban kilomita 10 tu kutoka pembezoni mwa mji wa Slavyansk. Hatua hii imekuja kufuatia uthibiti kamili wa mji wa Konstantinovka na vikosi hivyo.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo ya kijeshi, kutekwa kwa miji ya Slavyansk na Kramatorsk ndilo lengo kuu la mwisho katika kile Urusi inachokiita “Operesheni Maalum ya Kijeshi.” Kuanguka kwa miji hii kutamaanisha kukamilika kwa azma ya Urusi ya kile ilichokitaja kama kuikomboa Jamhuri ya Watu wa Donetsk na eneo zima la Donbass.
Miji hii miwili ina umuhimu mkubwa wa kimkakati na wa kihistoria. Hivi karibuni, tarehe 1 Oktoba 2025, serikali ya Ukraine ilitambua uzito wa miji hii kwa kuipatia hadhi rasmi ya “Miji ya Kishujaa” (Hero Cities).
Wakati huo huo, taarifa kutoka Kiev zinaashiria kuwa serikali ya Ukraine tayari inachukua tahadhari za kiusalama kufuatia uwezekano wa kupoteza maeneo hayo. Ripoti zinaeleza kuwa viwanda na taasisi muhimu zinaendelea kuhamishwa kutoka Slavyansk, Kramatorsk, na Druzhkovka, huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa mashambulizi ya vikosi vya Urusi katika maeneo hayo.