KUWAIT – Siri imefichuka kuhusu operesheni hatari iliyotekelezwa na marubani wa Iran, ambayo imeacha maswali mengi kuhusu uwezo wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani.

Mapema mwezi uliopita, vyombo vya habari vya kimataifa nchini Marekani, vikiwemo NBC, Washington Post, na Forbes, viliripoti tukio la kushangaza ambapo ndege za kivita za Iran aina ya F-5 — ambazo ni za teknolojia ya zamani — zilifanikiwa kupenya mifumo ya ulinzi wa anga na kushambulia Kambi ya Camp Buehring nchini Kuwait, muda mfupi baada ya kuanza kwa mgogoro.

Sasa, marubani waliohusika katika operesheni hiyo wameibuka na kuelezea jinsi walivyotekeleza shambulio hilo la kishujaa na lenye hatari kubwa.

Akisimulia tukio hilo, kamanda aliyekuwa akiongoza operesheni hiyo alisema kuwa baada ya kugundua kuwa nchi yao imeshambuliwa, waliamua kujibu mapigo mara moja kwa kulenga kambi hiyo ya Marekani.

“Tuliruka kwa umbali wa chini sana kutoka ardhini (low altitude). Tulikuwa tukiwajibika kupita chini ya nyaya za umeme wa msongo mkubwa na wakati mwingine tulikuwa tukiruka chini ya futi 50,” alieleza kamanda huyo.

Aliongeza kuwa licha ya kufahamu kuwa eneo hilo lilikuwa likilindwa na mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga, walikataa kukata tamaa. “Tulidumisha ukimya kamili wa mawasiliano ya redio (radio silence). Tulivuka maeneo ya maji ya nchi jirani na kuruka chini kiasi kwamba wakati mwingine tulijikuta tukipita katikati ya meli mbili zilizokuwa zimesimama baharini.”

Kulingana na marubani hao, walipoingia katika anga ya Kuwait, waliongeza kasi na kufika kambini hapo, ambapo walitumia mabomu ya kawaida (unguided free-fall bombs) ambayo yalihitaji usahihi wa hali ya juu na ukaribu na lengo kabla ya kuyashusha.

Shambulio hilo lilisababisha taharuki kubwa. Ripoti zinaeleza kuwa mifumo ya ulinzi ya Kuwait ilichanganyikiwa na kuanza kushambulia kimakosa ndege tatu za Marekani aina ya F-15. Kwa mujibu wa kamanda huyo, walitumia mbinu za kijasusi za kuwapoteza maadui (deception operation), hatua iliyowawezesha kuepuka kufuatiliwa na kutua salama katika eneo walilopanga.

“Hatukudhani kuwa tutarejea tukiwa hai,” alikiri mmoja wa marubani walioshiriki shambulio hilo, akiongeza kuwa alishuhudia vifaa vya kijeshi vya Marekani vikiteketea kwa moto baada ya mabomu yao kulipuka.

Operesheni hiyo yote ilichukua dakika 50 pekee, na ilikuwa ikijulikana na watu wachache sana kabla ya kutekelezwa.

Katika tukio jingine linalohusiana na oparesheni hiyo, ndege mbili za kivita za Iran aina ya Sukhoi Su-24 zilijaribu kufanya shambulio sawa na hilo katika Kambi ya Anga ya Al Udeid nchini Qatar. Hata hivyo, jaribio hilo halikufua dafu kwani ndege hizo ziligunduliwa na kutunguliwa na ndege ya kivita ya Qatar aina ya F-15EX Eagle II.

Ingawa hatma ya marubani wa ndege hizo za Sukhoi bado haijajulikana, mabaki ya ndege hizo yaliokolewa baharini na walinzi wa pwani wa Qatar.

Leave a Reply