Kiongozi Mkuu wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ametembelea kituo kipya cha uzalishaji wa vifaa vya nyuklia ambacho kimeanza kufanya kazi rasmi, na kutoa wito wa kuongezwa kwa kiwango kikubwa uwezo wa taifa hilo wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Kim amesema uwezo wa Korea Kaskazini wa kuzalisha vifaa vya nyuklia vinavyotumika kutengeneza silaha umeongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Pia amewaagiza maafisa husika kuongeza zaidi uzalishaji huo ili kusaidia utekelezaji wa malengo ya kimkakati ya muda mrefu ya nchi hiyo.
Wakati wa ziara hiyo, kiongozi huyo alipitia teknolojia mpya za uzalishaji, kiwango cha sasa cha uzalishaji pamoja na mipango ya baadaye ya maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, Kim alisisitiza kuwa kuongezeka kwa vitisho vya kiusalama na kile alichokielezea kama mvutano wa muda mrefu dhidi ya mataifa yenye uhasama kunalazimu Korea Kaskazini kuendelea kuimarisha uwezo wake wa kujihami kwa kutumia silaha za nyuklia kama njia ya kuzuia mashambulizi kutoka kwa maadui wake.