Bosnia na Herzegovina — Uchunguzi uliochapishwa na The Guardian unadai kuwa AAFS Infrastructure and Energy, kampuni isiyojulikana sana inayoripotiwa kuwa na uhusiano na watu wa karibu na Rais wa Marekani Donald Trump, iko katika hatua za mwisho za kupata mikataba ya nishati yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 1 nchini Bosnia na Herzegovina.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mradi unaotarajiwa kujumuishwa kwenye mikataba hiyo unahusisha ujenzi wa bomba kubwa la gesi linalolenga kupunguza utegemezi wa nchi hiyo kwa gesi kutoka Urusi.
Hata hivyo, wakosoaji wamenukuliwa wakieleza wasiwasi kwamba AAFS haina historia iliyothibitishwa ya kusimamia miradi mikubwa ya kiwango hicho, na kwamba ilichaguliwa bila kufanyika mchakato wa zabuni ya ushindani.
Uchunguzi huo pia unataja kuwa miongoni mwa wawakilishi wa kampuni hiyo ni wakili Jesse Binnall anayehusishwa na Trump, pamoja na Joe Flynn, ndugu wa aliyekuwa Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Michael Flynn.