Jtt, 2 Novemba 2026

Utaridi CI Media

Habari Ndani ya Sayari.

Maseneta Marekani Wamtaka Trump Afute Makubaliano ya Dizeli ya Urusi

Rais wa Marekani Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump anakabiliwa na upinzani kutoka ndani ya vyama vya Republican na Democratic baada ya kufikia makubaliano na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu usambazaji wa mamilioni ya tani za dizeli ya Urusi kwa Marekani na soko la kimataifa.

Maseneta saba wa Marekani, wakiwemo Warepublican wanne na Democrats watatu, wametaka utawala wa Trump kubadili mara moja uamuzi huo, wakisema unakinzana na sheria ya Marekani iliyopitishwa mwaka 2022 kuzuia uagizaji wa nishati kutoka Urusi.

Wabunge hao wamesema hatua hiyo inaweza kuipa Moscow kile walichokiita “njia ya kifedha ya kujiokoa”, wakati vita vya Urusi na Ukraine vikiendelea. Pia wameikosoa Ikulu ya White House kwa kutowasiliana na Congress kabla ya kuchukua uamuzi huo.

Sheria ya mwaka 2022 ilipitishwa kwa lengo la kuzuia fedha za Marekani kuingia Urusi kupitia biashara ya nishati, kama sehemu ya juhudi za Washington za kuipunguzia Moscow mapato yanayoweza kusaidia kufadhili vita nchini Ukraine.

Trump alitangaza makubaliano hayo Ijumaa baada ya mazungumzo ya simu na Putin ambayo aliyataja kuwa “yenye mafanikio makubwa.” Kwa mujibu wa mpango uliotangazwa, Urusi inatarajiwa kutoa zaidi ya tani 300,000 za dizeli mara moja, tani 500,000 mwezi Novemba na tani milioni moja baadaye, huku kiasi kingine kikitarajiwa kufuata.

Trump amesema hatua hiyo inalenga kuongeza usambazaji na kusaidia kupunguza bei za mafuta kwa Wamarekani.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa sekta ya nishati wameeleza mashaka kuhusu athari zake, wakisema kiasi cha mafuta kitakachoingia sokoni kinaweza kuwa kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya jumla ya dizeli duniani na hivyo kutokuwa na uwezo mkubwa wa kushusha bei kwa kiwango kinachoonekana.

Mvutano huo sasa unaweka suala la bei za nishati dhidi ya sera ya Washington ya kuiwekea Moscow shinikizo la kiuchumi, huku Trump akitetea mpango huo kama hatua ya kupunguza gharama za mafuta na wakosoaji wake wakisema unaweza kuipatia Urusi mapato mapya.

Chanzo: Reuters, Financial Times

Maoni

Maoni