Jtt, 19 Oktoba 2026

Utaridi CI Media

Habari Ndani ya Sayari.

,

Mkono wa Chuma wa Aliyev Dhidi ya Hijab: Je, Azerbaijan Inajifunga kwenye Mtego wa Magharibi?

Ilham Aliyev, rais wa Azerbaijan, katika picha ya kumbukumbu.

Mvutano mkubwa umezuka nchini Azerbaijan kufuatia sera mpya zinazoweka vizuizi vya uvaaji wa hijab shuleni. Hatua hii imesababisha wimbi kubwa la maandamano na kampeni za kijamii za kuwaunga mkono wasichana wanaovaa hijab, huku mamlaka zikijibu kwa ukali kwa kuwakamata watu 37 na kuweka vizuizi kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram na TikTok katika jaribio la kuzima habari hizo.

Mgogoro huo haujabakia ndani ya mipaka ya Azerbaijan pekee, bali umezua radiamali kali kutoka nchi jirani ya Uturuki. Rais Recep Tayyip Erdogan ameonyesha kuguswa na kadhia hiyo, ambayo imerejesha kumbukumbu za uchungu za marufuku ya hijab ya huko nyuma nchini Uturuki. Wachambuzi wengi wameanza kulinganisha sera za sasa za Rais Ilham Aliyev na zile za Ufaransa zinazokandamiza alama za kidini, huku wengine wakimlinganisha na baba yake katika mfumo wa uongozi.

Hali hii inaashiria mgogoro mkubwa wa kisiasa na kijamii unaohatarisha uhusiano wa kimkakati kati ya Baku na Ankara. Wakati wananchi wakipigania haki yao ya kidini na utambulisho, serikali ya Azerbaijan inakabiliwa na mtihani mgumu wa ima kuheshimu matakwa ya wananchi wake au kuendelea na mkondo wake wa kilasiki unaoungwa mkono na nchi za Magharibi, hatua inayozidi kuichochea mivutano ya kijiografia katika eneo la Caucasus haswa kwenye nchi hiyo ambayo zaidi ya asilimia 90 ni waislamu.

Maoni

Maoni