Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Seyed Abbas Araghchi, amesema kuwa matukio ya karibuni katika Mlango wa Bahari wa Hormuz yameweka wazi tena kwamba hakuna suluhisho la kijeshi kwa mgogoro wa kisiasa unaoikumba kanda ya Asia Magharibi, akisisitiza upya sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya kufuatilia diplomasia kutoka katika nafasi ya nguvu.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X usiku wa Jumatatu, Araghchi ameeleza kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yanaendelea kupiga hatua kwa uthabiti, huku akizipongeza juhudi za Pakistan kwa upatanishi wake wa dhati na wenye kujenga.

Amesema: “Mazungumzo yanapoendelea kupata mafanikio kutokana na juhudi za Pakistan, Marekani inapaswa kuwa makini isije ikavutwa tena katika dimbwi la matatizo na wale wasiolitakia mema eneo hili. Vivyo hivyo kwa Umoja wa Falme za Kiarabu.”

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran pia amekosoa vikali kile ambacho Washington imekuwa ikikitangaza sana kama “Mradi wa Uhuru” wenye lengo la kuongeza mashinikizo ya kijeshi katika Mlango wa Hormuz na ameutaja mpango huo kuwa “ Mradi wa Mkwamo.”

Kauli za Araghchi zinakuja wakati ambapo Jamhuri ya Kiislamu, kupitia uwezo wake wa kujihami na udhibiti wake thabiti katika njia hiyo ya kimkakati ya baharini, imeweza kuthibitisha kwamba jaribio lolote la kutaka kulazimisha matokeo kwa nguvu au vitisho halitaweza kufanikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *