Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

JUBA — Rais Salva Kiir ametia saini marekebisho ya sheria ya uchaguzi yanayoondoa masharti yaliyokuwa yakihusisha kufanyika kwa uchaguzi na kukamilika kwa katiba ya kudumu pamoja na sensa ya kitaifa, miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa Desemba 22.

Serikali inasema mabadiliko hayo yanaondoa vikwazo vya kisheria na kuweka mazingira ya kuendelea na uchaguzi ambao umeahirishwa mara kadhaa.

Hata hivyo, South Sudan Opposition Alliance (SSOA), muungano wa vyama vya upinzani na mmoja wa waliotia saini makubaliano ya amani ya 2018, umeyakataa marekebisho hayo, ukisema yalifanywa bila mashauriano ya kutosha kati ya pande za makubaliano hayo.

Sheria iliyorekebishwa pia inaruhusu uongozi uliopo madarakani kuendelea kutumia mamlaka yake ya kikatiba katika kipindi cha uchaguzi hadi rais atakayechaguliwa atakapoingia madarakani.

Sudan Kusini haijawahi kufanya uchaguzi mkuu tangu ilipopata uhuru mwaka 2011. Ikiwa uchaguzi wa Desemba utafanyika kama ulivyopangwa, utakuwa wa kwanza katika historia ya taifa hilo.

Maoni