Marekani imeibuka kuwa nchi pekee ulimwenguni iliyopiga kura ya kupinga azimio la Umoja wa Mataifa (UN) linaloidhinisha matumizi ya ramani mpya ya dunia inayolenga kuonyesha ukubwa halisi wa kijiografia wa mabara yote.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 164 za kuunga mkono, huku nchi sita zikijizuia, na kuifanya Marekani kubaki pweke katika msimamo wake wa kupinga mabadiliko hayo ya kihistoria.
Mpango huo unapitisha mfumo wa ramani unaojulikana kama Equal Earth projection, ambao unarekebisha upotoshaji mkubwa uliodumu kwa karne nyingi kupitia ramani ya jadi ya Mercator. Ramani ya Mercator, iliyobuniwa karne ya 16, ilikuwa ikiikuza Marekani ya Kaskazini na Bara la Ulaya kimuonekano huku ikilifanya bara la Afrika kuonekana dogo mno kuliko ukubwa wake halisi.
Kihalisia, Afrika ina eneo la kilomita za mraba zaidi ya milioni 30.3, eneo ambalo linaweza kumeza Marekani, China, India, na sehemu kubwa ya bara la Ulaya kwa pamoja.
Hatua hii ya Umoja wa Mataifa inatajwa na wachambuzi kama ushindi mkubwa katika ukombozi wa maarifa na fikra za kijiografia kwa Mataifa ya Kusini (Global South), huku kura ya pekee ya Marekani ikitazamwa kama jaribio la kutetea ishara za zamani za utawala wa kitamaduni na kisaikolojia.