WASHINGTON, MAREKANI — Seneta wa Republican Thom Tillis amemtaka Rais Donald Trump kumwondoa Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth, akimshutumu kwa usimamizi mbovu na kusababisha ombwe la uongozi katika jeshi la Marekani.
Tillis amesema hajawahi kushuhudia “usimamizi usio na uwezo” wa kiwango hicho dhidi ya wanaume na wanawake wanaolitumikia jeshi la Marekani. Pia amemshutumu Hegseth kwa kujikita katika migogoro ya kisiasa na kiutamaduni badala ya masuala muhimu ya ulinzi wa taifa.
Wito huo umetolewa baada ya Daniel Driscoll kujiuzulu kama Katibu wa Jeshi la Nchi Kavu, kufuatia miezi kadhaa ya mvutano ulioripotiwa kati yake na Hegseth. Tillis amesema kuondoka kwa viongozi wenye uzoefu kunazidisha ombwe katika safu za juu za jeshi.
Tillis, ambaye mwaka 2025 alipiga kura kuthibitisha uteuzi wa Hegseth, sasa amemtaka Trump kutafuta kiongozi mpya wa Pentagon ambaye, kwa maelezo yake, atawahifadhi na kuwawezesha wataalamu wa kijeshi badala ya kuwadhoofisha.
Ukosoaji huo unakuja wakati Pentagon ikiwa chini ya shinikizo kutokana na vita vinavyoendelea dhidi ya Iran, kupungua kwa baadhi ya akiba za silaha na mabadiliko ya mara kwa mara katika uongozi wa kijeshi.