JERUSALEM – Katika hali inayozua mjadala mzito nchini Israel, utafiti mpya wa kura ya maoni umebaini kuwa idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo wanaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea katika mzozo wa hivi karibuni unaoihusisha Israel na mshirika wake mkuu, Marekani.
Utafiti huo uliotekelezwa na Chuo Kikuu cha Hebrew (Hebrew University) kwa kushirikiana na Maabara ya Agam, unaonyesha kuwa asilimia 92 ya Waisraeli wanaamini kuwa Iran ndiye mshindi wa kweli katika mvutano huo.
Matokeo hayo yanaashiria kutoridhishwa kwa umma na makubaliano yaliyofikiwa wiki hii kati ya Marekani na Iran, ambayo yanajumuisha pia usitishaji vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebanon. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sehemu kubwa ya Waisraeli wanaona makubaliano hayo kuwa ni pigo kwa maslahi ya nchi yao.
Usalama wa Taifa Mashakani
Aidha, kura hiyo ya maoni imefichua hofu kubwa ya kiusalama miongoni mwa raia. Takriban asilimia 82.9 ya waliohojiwa wamesema wanaamini kuwa kampeni ya kijeshi dhidi ya Iran badala ya kuimarisha nchi, imedhoofisha usalama wa muda mrefu wa Israel. Vilevile, asilimia 86 ya wananchi wameonyesha kuwa na mtazamo hasi kuhusu matokeo ya jumla ya mzozo huo.
Imani kwa Netanyahu Yaporomoka
Katika hatua nyingine, utafiti huo umeonyesha kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Licha ya kiongozi huyo kusisitiza kuwa nchi yake imepata mafanikio makubwa na kuondoa tishio la kuangamizwa kwa taifa la Israel, asilimia 72.5 ya raia wamesema hawamuamini.
Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa matokeo haya ni kielelezo cha mgawanyiko mkubwa na kutoaminiana kati ya serikali na umma, huku raia wengi wakionekana kuwa na wasiwasi juu ya hatma ya usalama wa nchi yao kufuatia makubaliano hayo ya kimataifa.