TEHRAN – Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imethibitisha rasmi kufikiwa kwa makubaliano muhimu kati ya Iran na Marekani, baada ya Marais wa mataifa yote mawili, Masoud Pezeshkian na Donald Trump, kutia saini mkataba wa maelewano (MoU) kwa njia ya kielektroniki.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema hatua hiyo inaifanya makubaliano hayo kuwa ya kisheria na yenye nguvu.
Licha ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, hakutakuwa na sherehe yoyote rasmi ya utiaji saini siku ya Ijumaa. Badala yake, pande zote mbili zimekubaliana kuanza awamu ya kwanza ya mazungumzo ya kiufundi ya siku 30 kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo. Ujumbe wa Iran utaongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Qalibaf, wakati Marekani itawakilishwa na Makamu wa Rais, JD Vance. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika nchini Uswisi.
Kipaumbele cha Usitishaji Mapigano Lebanon
Katika hatua nyingine, imebainika kuwa nchi ya Lebanon imetajwa mara tatu katika kifungu cha kwanza cha mkataba huo, hatua inayolenga kusisitiza heshima kwa uhuru na mamlaka ya ardhi ya nchi hiyo. Baghaei amesisitiza kuwa kufikiwa kwa usitishaji wa mapigano nchini Lebanon kulikuwa na umuhimu sawa kwa Tehran kama ilivyokuwa kwa masharti mengine yanayohusu Iran moja kwa moja.
Meli za Iran Zaanza Safari Huru
Kuhusu hatua za awali za utekelezaji, msemaji huyo ameeleza kuwa meli za Iran zimeanza kusafiri kwa uhuru katika bandari mbalimbali. Baghaei ameelezea hali hii kama matokeo ya awali ya ahadi ya Marekani ya kuondoa kizuizi cha majini (naval blockade) ambacho kimekuwa kikiathiri shughuli za usafirishaji wa Iran.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, majukumu ya Iran chini ya makubaliano hayo, ikiwemo yale yanayohusiana na usalama katika Lango la Hormuz, yameanza kutekelezwa rasmi mara tu baada ya kusainiwa kwa mkataba huo.